The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

DKT.HOMERA AWASILI WIZARA YA N...

DKT.HOMERA AWASILI WIZARA YA NISHATI; ATAKA KASI NA WELEDI KATIKA UTENDAJI

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amewataka viongozi na watumishi wa Wizara ya Nishati kuongeza kasi na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora kupitia sekta ya nishati.

Dkt. Homera amesema hayo leo, Oktoba 1, 2026, mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Wizara ya Nishati, Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, kufuatia kuapishwa kwake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Alipowasili Wizarani, Dkt. Homera alipokelewa na viongozi na watumishi wa Wizara pamoja na watendaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara, wakiongozwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba.

Akizungumza na viongozi na watumishi hao, Dkt. Homera amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa kasi, weledi na ushirikiano ili kuendelea kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi na kusukuma mbele maendeleo ya sekta ya nishati nchini.

Aidha, ameahidi kushirikiana kwa karibu na viongozi, watendaji na watumishi wa Wizara pamoja na taasisi zake katika kutekeleza majukumu na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo.

Dkt. Homera pia amepongeza kazi iliyofanyika hadi sasa katika sekta ya nishati, hususan utekelezaji wa miradi mbalimbali, huku akiwataka watumishi kumpa ushirikiano ili kuendeleza kasi ya utekelezaji wa shughuli na miradi hiyo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amemhakikishia Dkt. Homera ushirikiano kutoka kwa viongozi, watendaji na watumishi wa Wizara pamoja na taasisi zake katika kutekeleza majukumu yake.