TANESCO NA CRDB KULETA MAPINDUZI KATIKA UUNGANISHAJI WANANCHI NA UMEME – MGALU
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, amesema mpango maalumu wa kuharakisha uunganishaji wa umeme katika kaya unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Benki ya CRDB unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika huduma ya kuwaunganishia wananchi umeme nchini.
Mhe. Mgalu ameyasema hayo leo Novemaba 23, 2026 wakati wa semina ya kujenga uelewa na uzoefu kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hyatt Regency Kilimanjaro Hotel jijini Dar es Salaam.
Amesema ubunifu huo wa ushirikiano kati ya TANESCO na CRDB ni sehemu ya kuendeleza utekelezaji wa mkakati wa Mission 300, unaolenga kuwawezesha zaidi ya watu milioni 300 barani Afrika kupata huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030.
Aidha, amesema mpango huo maalumu umeweka msisitizo katika kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kuunganishiwa umeme bila vikwazo vinavyotokana na hali zao za kiuchumi.
Ameeleza kuwa baada ya Kamati kuona umuhimu wa mpango huo, iliamua kuwasilisha ombi la kupatiwa mafunzo ili kupata uelewa wa kina kuhusu namna utakavyotekelezwa, utendaji wake na manufaa yake kwa wananchi.
Amesisitiza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati hiyo kuelewa vyema mpango huo na kuwa na uwezo wa kutoa elimu kwa wananchi katika majimbo yao kuhusu fursa na namna ya kunufaika na mpango wa uunganishaji umeme.