The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

DKT. MATARAGIO NA KATIBU MKUU...

DKT. MATARAGIO NA KATIBU MKUU WA PETROLI ZAMBIA WAJADILI MIKAKATI YA USHIRIKIANO SEKTA YA MAFUTA.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio, leo Novemba 11, 2026, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Wizara ya Petroli ya Zambia, ukiongozwa na Katibu Mkuu, Prof. Ephraim Munshifwa, kuhusu kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta ya mafuta.

Kikao kati ya pande hizo mbili kimefanyika jijini Dar es Salaam kikijikita katika kujadili kwa kina masuala mbalimbali yenye maslahi ya pamoja katika sekta hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza uhusiano wa kiuchumi na ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Zambia katika kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wananchi.

Tanzania na Zambia zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu katika sekta ya mafuta kupitia Bomba la Mafuta la TAZAMA, huku nchi hizo zikiendelea na mipango ya kupanua ushirikiano katika maeneo mengine.

Ujumbe wa Zambia umejumuisha Wakurugenzi mbalimbali kutoka Ofisi ya Rais, Wizara ya Petroli, Wizara ya Fedha na Wizara ya Sheria, huku kwa upande wa Tanzania kikao hicho kikihudhuriwa na Msajili wa Hazina, Ndg. Nehemia Mchechu, Kamishna wa Petroli, Godluck Shirima, watendaji kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).