Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Jamii yatakiwa kutunza mazing...

​Jamii yatakiwa kutunza mazingira kuzunguka mabwawa ya umeme.

Jamii yatakiwa kutunza mazingira kuzunguka mabwawa ya umeme.

Na Timotheo Mathayo, Iringa.

Jamii inayozunguka mradi wa bwawa la kufua umeme la Kihansi lililopo mkoani Iringa wametakiwa kulinda na kutunza mazingira ili mradi huo uwe endelevu kwa manufaa ya taifa.

Kauli hiyo imetolewa jana na Naibu waziri wa nishati, Steven Byabato alipotembelea bwawa hilo kuona hali halisi ilivyo ambapo kutokana na kujaa maji, amewahakikishia wananchi kwamba maji yaliyopo yanatosha kuzalisha umeme.

Byabato yupo katika ziara ya kukagua mradi wa bwawa la kuzalisha umeme wa Kihansi ambapo alisema ameridhishwa na kiwango cha maji kinachotokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali.

Mradi wa Kihansi una uwezo wa kuzalisha umeme megawati 180 kutoka kwenye mitambo mitatu ambapo kila mtambo unazalisha megawati 60.

“Mwisho wa mwaka jana (2021) Taifa lilipata shida ya umeme kwa sababu maji yalipungua kwenye mabwawa ya kufua mitambo ya kuzalisha umeme ya Ruvu, Kidatu na Kihansi, na tukumbuke Waziri wa Nishati, Januari Makamba alifika kuona hali halisi," alisema Byabato.

Alisema amefanya ziara hiyo baada ya kutumwa na Waziri wa Nishati ili kuona mambo yalivyo kwenye mabwawa ya kufua umeme.

Maji katika bwawa la Kihansi yamefikia ujazo wa mita 1,145 kati ya mita 1,147 kutoka usawa wa bahari, hivyo kiwango cha maji yaliyopo kinatosha kuzalisha umeme.

Alisema wataalam wamemuhakikishia kwamba endapo mvua zitaendelea kunyesha hadi mwezi wa pili mwaka huu katika mikoa ya Iringa na Morogoro, shirika la umeme nchini, Tanesco litakuwa na uwezo wa kusambaza umeme kwa uhakika hadi mwezi wa nane au tisa mwaka huu.

Aidha akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua mradi huo, Byabato alitaja bwawa la Kidatu kama mradi mkubwa kwani linazalisha umeme megawati 200 ambazo huunganishwa katika gridi ya taifa.

Baadhi ya changamoto zilizobainika wakati wa ziara hiyo ni pamoja na watu kufanya shughuli za kilimo jiranii na vhanzo vya maji, jambo ambalo linatishia uharibifu wa mazingira na hivyo maji kupungua kiasi cha kuathiri uzalisha wa umeme nchini.

Umeme unaozalishwa bwawa la Kihansi lililopo Iringa na mitambo yake ya kufua umeme ikiwa mkoani Morogoro unaunganishwa kwenye gridi ya Taifa na unatumika katika mikoa yote inayotumia umeme wa gridi ya taifa.

Hata hivyo Byabato alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Wizara ya Nishati ili itekeleze majukumu yake ya Kila siku kwa ufanisi mkubwa.