Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Kamati ya Bunge ya Hesabu za...

​Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali yapata elimu ya Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali yapata elimu ya Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja

Na Ruben Richard

Wajumbe wa Kamati Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wamepata elimu kuhusu shughuli za Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja zinazosimamiwa na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amesema kuwa lengo la kutoa elimu hiyo ni kuwawezesha Wajumbe hao kufahamu kwa kina kuhusu utendaji wa Taasisi ya PBPA iliyopewa jukumu la kusimamia shughuli za uagizaji wa mafuta kwa pamoja.

Semina hiyo imefanyika jijini Dodoma tarehe 6 Novemba, 2022 na kuhudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PBPA, Erasto Mulokozi, aliieleza Kamati hiyo kuhusu historia ya shughuli za uagizaji wa mafuta nchini pia kazi zinazofanywa na taasisi hiyo kwa sasa za uagizaji na upokeaji wa mafuta.

Amesema kuwa, kutoka Wakala huo uanzishwe mwaka 2015 umekuwa na mafanikio mbalimbali ikiwemo kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta yanayotosheleza mahitaji na yenye viwango vya ubora unaohitajika.

Manufaa mengine ni Serikali kuweza kupanga ukusanyaji wa mapato kwa kuzingatia takwimu sahihi, kuweza kupanga bei elekezi ya mafuta pamoja na kupata unafuu wa gharama za uletaji wa mafuta nchini kutokana na uagizaji wa mafuta kwa pamoja kwa wastani wa zaidi ya Dola. za Marekani milioni 200 Sawa na shilingi bilioni 462 huokolewa kwa mwaka.

Aidha amesema kuwa, kutokana na mfumo huo kuleta ufanisi, nchi za jirani pia zinatumia mfumo huo kuagiza mafuta kupitia Tanzania hivyo kuipatia Serikali mapato kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya bandari.

Ameongeza kuwa, mfumo huo umesaidia kupunguza upotevu wa mafuta wakati wa kupakua mafuta kutoka melini ambapo wastani wa Tani 1100 ( lita 1,300,000) huokolewa kila mwezi sawa na shilingi bilioni 4.3.

Wajumbe wa Kamati hiyo walipongeza kuhusu mfumo ambao umeonesha ufanisi, ambapo pia Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Mhe. Naghenjwa Kaboyoka ameishukuru Wizara ya Nishati kupitia PBPA kwa kupata uelewa huo ambao umesaidia Kamati kufahamu Sekta pamoja na changamoto zake.

Vilevile, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali ametoa wito kwa Wajumbe wa Kamati hiyo kuendelea kutoa ushauri na maelekezo ambayo yataiwezesha Sekta ya Nishati kuendelea kuendeshwa kwa ufanisi.