Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA KASI...

KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA KASI YA UJENZI WA KIWANDA CHA MABOMBA MRADI WA EACOP

KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA KASI YA UJENZI WA KIWANDA CHA MABOMBA MRADI WA EACOP

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imepongeza kasi ya ujenzi wa kiwanda kitakachokuwa kikiweka mifumo ya upashaji jotona plastiki itakayozuia upotevu wa joto kwenye mabomba yatakayotumika katika mradiwa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Hayo yameelezwa tarehe 26 Agosti, 2023 na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe.Judith Kapinga katika Kijiji cha Sojo, wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora wakati wajumbe wa Kamati hiyo walipofika kiwandani hapo kujionea utekelezaji wake.

Mara baada ya kukagua kazi mbalimbali zinazoendelea katika kiwanda hicho ambacho ujenzi wake kwa ujumla umefikia asilimia 95, Mhe. Kapinga aliipongeza Serikali kwa utekelezaji huo ambapo pia amesifu teknolojia ya hali ya juu inayotumika katika kiwanda hicho.

“Kamati imeridhishwa na maendeleo ya mradi huu ambao kwa kweli unatekelezwa kwa kasi nzuri, nichukue fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa ujumla kwa kuendelea kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa ipasavyo.” Amesema Mhe.Kapinga

Sanjari na hayo, Mhe.Kapinga ametoa wito kwa Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi hasa wanaozunguka miradi mbalimbali inayoendelea chini ya EACOP kuhusu fursa zinazotokana na miradi hiyo, huduma za kijamii na kuhakikisha kuwa mahusiano chanya na wananchi wanaozunguka miradi yanaendelea kuwepo ili miradi hiyo ifanyike kwa ufanisi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato pamoja na kueleza hatua zinazoendelea kufanyika katika mradi wa EACOP ikiwemo ujenzi wa kiwanda hicho na kambi mbalimbali zitakazotumika kwa ajili ya wafanyakazi na kuhifadhi vifaa vitakavyotumika wakati wa utekelezaji mradi, alisema kuwa Serikali pia inaendelea kusimamia kwa umakini suala la utoaji wa huduma za kijamii katika maeneo ambapo mradi unapita.

Byabato amewashukuruWajumbe wa Kamati kwa kufanya ziara hiyoili kujionea jinsi Serikali inavyoendelea kutekeleza mradi wa EACOP na kuahidi kuwa maoni mbalimbali yaliyotolewa na Wajumbe hao yatafanyiwa kazi na Serikali ili kuendelea kuboresha utekelezaji wa mradi wa EACOP.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitwapaki Tukai, amesema kuwa, utekelezaji wa mradi huo unaenda vizuri na kumekuwepo na ushirikishwaji mzuri wa jamii inayozunguka mradilengo likiwa ni kuhakikisha kuwa wanafaidika na uwepo wa kiwanda hicho katika eneo la Sojo.

Viongozi mbalimbali waliohudhuria ziara hiyo ni Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitwapaki Tukai, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mussa Makame, Mratibu Mradi wa EACOP upande wa Tanzania, Asiad Mrutu na Mratibu Mradi wa EACOP katika Wizara ya Nishati, Kisamarwa Nyang’au.