The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

KAMATI ZA MAADILI ZATAJWA KUWA...

KAMATI ZA MAADILI ZATAJWA KUWA NGUZO YA KUBADILI TABIA ZA WATUMISHI.

Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala (ADA), Wizara ya Nishati, Bw. Wilson Nyamanga, amesema Kamati za Maadili zilizopo katika Wizara hiyo na taasisi zake zina nafasi muhimu katika kubadili tabia na mienendo ya watumishi na kuwawezesha kuzingatia misingi ya Utumishi wa Umma.

Bw. Nyamanga ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha Kamati ya Maadili ya Wizara ya Nishati na taasisi zake, kilichofanyika katika ukumbi wa Timeless Hotel, mjini Morogoro, Nyamanga akimuakikisha Mwenyekiti wa kamati Septemba 08,2026.

Amesema kamati hizo zimeanzishwa kwa lengo la kusaidia watumishi kuachana na tabia na mienendo isiyofaa na kuwa na mwenendo unaozingatia maadili, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma.

“Kamati hizi zinasaidia kubadilisha tabia na mienendo ya watumishi kutoka tabia zisizofaa kwenda kwenye tabia zinazofaa katika Utumishi wa Umma”. Amesema Bw. Nyamanga.

Ameeleza kuwa jukumu kubwa la Kamati ya Maadili ni kuangalia tabia na mienendo ya watumishi, kuwashauri na kuwasaidia kurekebisha mwenendo wao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya maadili ya Utumishi wa Umma.

Aidha, amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati kuhakikisha zinatoa mafunzo ya maadili kwa watumishi wapya mara wanapoajiriwa, ili kuwajengea uelewa kuhusu taratibu na maadili yanayoongoza Utumishi wa Umma.

Bw. Nyamanga amesisitiza kuwa mafunzo ya Utumishi wa Umma yanapaswa kwenda sambamba na elimu ya maadili, akieleza kuwa bila kuzingatia maadili, elimu hiyo haitakuwa na maana iliyokusudiwa.

“Ufundishaji wa Utumishi wa Umma bila ya maadili ya Utumishi wa Umma, bado hatujafanya kitu,” amesema.