Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​MAJADILIANO ‘HGA’ YANUKIA, WA...

​MAJADILIANO ‘HGA’ YANUKIA, WAZIRI MAKAMBA AKUTANA NA VIONGOZI EQUINOR

MAJADILIANO ‘HGA’ YANUKIA, WAZIRI MAKAMBA AKUTANA NA VIONGOZI EQUINOR

Na Janeth Mesomapya

Waziri wa Nishati Mh. January Yusuf Makamba amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa kampuni ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia ya Equinor (Afrika) Bw. Paul McCafferty.

Viongozi hao wamekutana Oktoba 21, 2021 katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati zilizopo jijini Dar es Salaam. Mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na viongozi wengine wa Equinor na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC).

Imeelezwa kuwa mazungumzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya majadiliano ya Mkataba wa Nchi Hodhi (HGA) wa Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) yanayotarajiwa kuanza rasmi Novemba 8, 2021.

Kwenye kikao hicho, Bw. McCafferty amempongeza Waziri Makamba kwa niaba ya serikali kwa hatua hiyo ya kuanza tena kwa majadiliano ya mkataba huo wa HGA kwani yatafungua njia kwaajili ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo wa LNG.

Bw. McCafferty ameeleza kuwa Equinor iko tayari kwa majadiliano hayo na kuongeza kwamba mradi huo ni moja ya miradi yenye uwekezaji mkubwa inayotekelezwa na Equinor duniani, hivyo ni majadiliano muhimu katika kuweka msingi mzuri wa utekelezaji wake.

Equinor ni moja ya wabia wakuu wa utekelezaji wa mradi huu wa LNG ambao utasimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA). Wabia wengine ni pamoja na kampuni ya Shell na TPDC kwa niaba ya serikali.

Mradi wa LNG unakadiriwa kuwa wa thamani ya takriban Dola za Marekani bilioni 30 huku ukitarajiwa kutengeneza nafasi za ajira za moja kwa moja 6,000 na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 15,000 kwa Watanzania.