MAMBAMIAMBA YAINGIA RASMI KATIKA SAFARI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA.
Wananchi wa Kata ya Mambamiamba, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Julai 30, 2026, wamejengewa uelewa kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia wakati wa hafla ya uzinduzi wa Tawi la Tanzania Women Empowerment Network (TAWEN).
Hafla hiyo imezikutanisha taasisi mbalimbali za Serikali, wadau wa maendeleo na wananchi, ambapo kila taasisi imepata fursa ya kuwasilisha huduma zake pamoja na kuelezea fursa zinazopatikana katika sekta zake. Wizara ya Nishati ilitumia fursa hiyo kutoa elimu kuhusu faida za matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwemo kulinda afya, kuhifadhi mazingira na kupunguza gharama za matumizi ya nishati.
Akiwasilisha mada, Mtaalamu kutoka Wizara ya Nishati, Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Mha. Benezeth Kabunduguru, amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 - 2034), unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, kutoka asilimia 28.6 mwaka 2025.
Amesema lengo hilo litafikiwa kupitia ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, wadau wa maendeleo na wananchi katika kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia na kuendelea kutoa elimu kuhusu faida za matumizi yake. Ameongeza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yanachangia kulinda afya za wananchi kwa kupunguza athari za moshi unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa, kuhifadhi mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti, pamoja na kuokoa muda na gharama zinazotumika katika shughuli za kupikia, hususan kwa wanawake na watoto.
Aidha, amewahimiza wananchi wa Kata ya Mambamiamba kuchangamkia matumizi ya teknolojia mbalimbali za nishati safi ya kupikia zinazopatikana nchini ili kuongeza matumizi ya nishati hiyo na kuunga mkono juhudi za Serikali za kufikia malengo ya Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWEN, Balozi Amina Salum Ali, ameipongeza Wizara ya Nishati na taasisi zake kwa kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia. Amesema juhudi hizo zinaongeza uelewa wa wananchi na kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi ya nishati.
Ameongeza kuwa TAWEN itaendelea kushirikiana na Wizara ya Nishati pamoja na wadau wengine kuhakikisha elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia inawafikia wanawake na jamii kwa ujumla ili kuongeza matumizi ya nishati hiyo kwa manufaa ya afya, mazingira na maendeleo ya kiuchumi ya wananchi.