Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​MHA. LUOGA AZINDUA UTAFITI WA...

​MHA. LUOGA AZINDUA UTAFITI WA MATUMIZI YA NISHATI KATIKA KAYA, WA MWAKA 2023.

Kamishina wa Umeme na Nishati Jadidifu Mha. Innocent Luoga kutoka Wizara ya Nishati , amezindua Takwimu za Matumizi ya Nishati katika Kaya kwa mwaka 2023.

Hafla hiyo imefanyika katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu leo tarehe 17 Novemba 2025 Jijini Dodoma.

Kamishina Luoga amefanya uzinduzi huo leo wakati akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mha. Felchesmi Mramba ambapo amesema kuwa tukio hilo ni hatua muhimu katika juhudi za Serikali kuhakikisha tunapata takwimu sahihi na za kuaminika kuhusu namna Watanzania wanavyotumia aina mbalimbali za Nishati majumbani mwao ikiwa ni pamoja na umeme, gesi, kuni, mkaa na Nishati jadidifu kama vile nishati ya umeme wa jua na Upepo

Vilevile, Kamishina ameeleza ripoti hiyo ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Wizara ya Nishati pamoja na taasisi zake, kwa ufadhili na usaidizi wa kiufundi na utaalam kutoka Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) kupitia Expertise France. Ameeleza“ Napenda kutoa pongezi kwa timu zote zilizoshiriki katika utafiti huu zilizoshirikisha wataalam wa takwimu na watafiti wa Nishati kwa kazi nzuri na ya kitaalam inayofanikisha kupatikana kwa ripoti hii muhimu”.

Aidha, Mha. Luoga amesema asilimia 52.7 ya kaya nchini zinatumia umeme kama chanzo cha Nishati. Hata hivyo, matokeo yanaonesha tofauti kubwa kati ya maeneo ya mjini na vijijini ambapo matumizi ya umeme mijini ni asilimia 72.7 wakati vijijini ni asilimia 30.7 pekee.

Sambamba na hilo Kamishina amesisitiza kuwa ripoti hii imebainisha kuwa asilimia 66 ya kaya hutumia kuni, asilimia 44 hutumia mkaa, wakati asilimia 25 inatumia gesi ya LPG, na asilimia 2 zinatumia umeme kwaajili ya kupikia. Hii inaonesha bado kuna nafasi kubwa ya kuelimisha na kuhamasisha Wananchi kuhusu matumizi ya Nishati safi na salama ya kupikia, ili kulinda afya, mazingira na rasilimali zetu za misitu.

Kwa upande wa Nishati kwa Maendeleo ya Viwanda Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa Umeme wa uhakika na wa gharama nafuu kupitia Miradi mikubwa ya kimakakati kama Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) ambalo limekamilika kwa asilimia 100 na kuwezesha upatikanaji wa umeme wa jua na upepo hivyo kusaidia kupanua mtandao wa gridi ya taifa ili kufikia viwanda vyote vidogo na vikubwa katika mikoa yote.

Kwa muktadha huo Mha. Luoga ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutumia matokeo ya Utafiti huu kama nyenzo muhimu katika kupanga na kutekeleza sera bora za Nishati, zinazolenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata Nishati ya uhakika, nafuu na endelevu.

Naye, Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Amina Msengwa ameishukuru Wizara ya Nishati na taasisi zake zote kwa ushirikiano wao kwa kipindi chote cha kuandaa takwimu hizi lakini pia amemwomba Kamishna wa umeme na Nishati Jadidifu Mha. Innocent Luoga kuwa miradi hii ya kuandaa ripoti za utafiti wa matumizi ya Nishati katika kaya iwe endelevu, kwani itatusaidia katika utekelezaji wa Sera na mikakati madhubuti.

Pia, Mhe. Anna Makinda, Spika Mstaafu na Kamisa wa Sensa 2022, ametoa shukrani za dhati kwa wageni wote walioshiriki katika uzinduzi wa Utafiti wa Matumizi ya Nishati katika Kaya amesema kupitia ripoti hii tunatakiwa kuchukua hatua kama tutafanikiwa kutumia nishati safi itatusaidia kutunza muda na mazingira yetu kwa ujumla.

“Naipongeza Wizara ya Nishati na Tasisi zake pamoja na wadau mbalimbali lakini pia Wananchi waliotoa taarifa hizi kwani itatusaidia kuongeza matumizi ya nishati safi na kuachana na Nishati zisizo salama”, Ameongeza Mhe. Makinda.

#NishatiTupokazini.