The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

NAIBU WAZIRI WA NISHATI APELEK...

NAIBU WAZIRI WA NISHATI APELEKA TABASAMU KWA MAMA MANYEMA.

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba (Mb), amemuwezesha mfanyabiashara, Bi. Afua Juma maarufu kama Mama Manyema, kuanza kutumia nishati safi ya kupikia katika shughuli zake za biashara ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa matumizi ya teknolojia hiyo, Mhe. Salome Makamba amesema hatua hiyo ilitokana na maombi aliyoyapokea kutoka kwa Mbunge wa Ubungo, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, ambaye alimweleza umuhimu wa kumwezesha Mama Manyema kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Amesema Bi. Afua Juma maarufu kama Mama Manyema si mfanyabiashara pekee, bali ni mtu aliyejijengea heshima kubwa katika jamii kupitia huduma anazozitoa. Ameongeza kuwa hatua yake ya kuanza kutumia nishati safi ya kupikia itakuwa mfano kwa wafanyabiashara wengine pamoja na wananchi kwa ujumla.

Mhe. Salome Makamba amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia, ambapo zaidi ya shilingi milioni 15 zimetumika kufanikisha uwekezaji wa mfumo wa teknolojia ya nishati safi ya kupikia kwa Mama Manyema.

Ameeleza kuwa hatua hiyo inaendana na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanahamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kulinda afya, mazingira na kuboresha ustawi wa wananchi.

Aidha, amemtaka Mama Manyema kuwa balozi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha wafanyabiashara pamoja na wananchi wengine kuachana na matumizi ya nishati zisizo safi na kuhamia kwenye nishati safi, akisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuona Watanzania wanabadilika na kukumbatia matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kwa upande wake, Bi. Afua Juma maarufu kama Mama Manyema, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Wizara ya Nishati kwa kumwezesha kupata teknolojia ya nishati safi ya kupikia. Amesema hatua hiyo itaongeza ufanisi katika biashara yake, kupunguza gharama za uendeshaji na kuboresha mazingira ya kazi.