NDEJEMBI ASISITIZA KASI YA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA KUSAFIRISHA UMEME KATIKA MIKOA YA LINDI NA MTWARA.
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya kimkakati ya usafirishaji wa umeme katika ukanda wa kusini kuongeza kasi ya utekelezaji ili kuwezesha mikoa ya Lindi na Mtwara kuunganishwa katika Gridi ya Taifa kwa kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika.
Ametoa maagizo hayo Julai 21 2026, katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Ujenzi wa Njia Maalum ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa Kilovolti 33 yenye urefu wa kilometa 76 kutoka Kituo cha Switching cha Masasi hadi Wilaya ya Newala.
“Serikali inatarajia kuona kazi zinaendelea kwa kasi, kwa kuzingatia viwango vya ubora ili wananchi waanze kunufaika na huduma ya umeme wa Gridi ya Taifa haraka iwezekanavyo,” amesisitiza Ndejembi.
Waziri Ndejembi amesema Serikali inaamini kuwa upatikanaji wa umeme wa uhakika ni msingi wa maendeleo ya Taifa, ndiyo maana inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya umeme ili kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma.
Akizungumzia uzinduzi wa Mradi wa Ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme, amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi na kuweka mazingira wezeshi kwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika Wilaya ya Newala.
Amesema Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika miradi ya kimkakati ya umeme ili kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana katika kila eneo la nchi, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi, kuvutia uwekezaji, kuongeza ajira na kuinua maisha ya wananchi.
Aidha, amesema Serikali kupitia TANESCO imeanza maandalizi ya utekelezaji wa mradi mwingine mkubwa wa Masasi hadi Mahumbika, unaohusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 220 yenye urefu wa kilometa 128, pamoja na ujenzi wa Kituo kipya cha Kupooza Umeme cha Mahumbika chenye uwezo wa 220/33kV na upanuzi wa Kituo cha Masasi.
Mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 33 wenye urefu wa kilometa 76 kutoka Masasi hadi Newala umegharimu shilingi bilioni 4.65 za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na tayari umeanza kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Wilaya ya Newala.