NDEJEMBI AZINDUA MKAKATI NA MPANGO KAZI WA MAGEUZI YA NISHATI UTAKAOTEKELEZWA NA NCHI ZA AFRIKA
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amezindua Mkakati na Mpango Kazi wa Mageuzi ya Nishati ambao utatekelezwa na Nchi za Afrika kupitia Kamisheni ya Nishati ya Afrika (AFREC).
Uzinduzi huo umefanyika leo Desemba 11, 2025 ikiwa ni muendelezo wa Kongamano la Nishati la Umoja wa Nchi za Afrika (AU) linalofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia na kushuhudiwa na Mawaziri wa Nishati wa Nchi za Afrika, Washirika wa Maendeleo na Wadau wa Nishati.
Katika uzinduzi huo, Mhe. Ndejembi ameeleza umuhimu wa Nchi za Afrika kutumia Nishati Safi katika kuzalisha umeme viwandani, majumbani, usafiri na majengo ili kutunza mazingira na kupunguza hewa ukaa ambapo kwa Afrika inakadiriwa kufikia asilimia nne.
Katika utekelezaji wa mkakati huo Mhe Ndejembi amezihimiza Nchi za Afrika kutumia vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme ili kuhakikisha kuwa watu milioni 600 barani Afrika wanafikiwa na huduma ya umeme.
" Tukiwa kama Viongozi wa Afrika tuna jukumu la kuhakikisha watu wetu wote wanapata huduma ya umeme ya uhakika. Tayari Tanzania kupitia mpango wa mission 300 tumejiwekea lengo la kuhakikisha ifikapo Mwaka 2030 watanzania wote wanapata huduma ya umeme ambapo hadi sasa tayari tumefikia asilimia 85," Amesema Mhe. Ndejembi.
Katika kongamano hilo, Mhe Ndejembi ameambatana na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga.