Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​SERIKALI KUUNDA KIKUNDI KAZI...

​SERIKALI KUUNDA KIKUNDI KAZI KUHUSU NISHATI YA KUPIKIA.

SERIKALI KUUNDA KIKUNDI KAZI KUHUSU NISHATI YA KUPIKIA.

Na Timotheo Mathayo, Dar es salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameelekeza Wizara ya Nishati kuunda kikudi kazi kwa ajili ya kupitia na kuchakata Sera zilizopo kwa ajili ya kuelekea kwenye mpango wa taifa kuondokana na matumizi ya gesi chafu ya kupikia ifikapo 2032.

Ametoa agizo hilo Jumanne Novemba 01, 2022 alipokuwa akifungua mjadala wa kitaifa kuhusu matumizi ya Nishati safi ya kupikia unaofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es salaam.

Kikudi kazi hicho kitaongozwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Nishati itaratibu na kufanya shughuli za sekretarieti za kikudi hicho.

Ili kuongeza tija na ufanisi Rais Samia ameagiza muundo wa kikudi kazi ujumuishe pamoja wataalam kutoka Idara na Taasisi za umma, pia wawepo watu kutoka sekta binafsi na wadau wengine wa mazingira.

"Kikudi kazi kikapitie Sera na miongozo mbalimbali ili kije na mpango mkakati na dira ya miaka kumi kikielekeza mambo muhimu ya kufanya ili ifikapo 2032 kila mtu atumie nishati safi ya kupikia," amesema Rais Samia.

Alisema kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yatasaidia wanawake kuondokana na adha ya kutafuta kuni porini ambapo wengi wao wapo kwenye hatari ya kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kushambuliwa wanyama wakali na nyoka.

Pia muda wanaoupoteza porini kutafuta kuni wautumie kwa kufanya shughuli za uzalishaji mali kama kufuma na kufanya biashara ndogo ndogo.

Ameahidi kuwa serikali katika bajeti ya mwaka 2023/2024 itatenga fedha kwa ajili ya kuanzisha mfuko wa nishati safi ya kupikia utakaoshughulikia masuala ya utafiti na uwekezaji katika kutatua changamoto zilizopo.

Rais Samia alisema takwimu zinaonyesha kuwa kaya zinazotumia gesi kupikia ni 5% na zinazotumia umeme ni 3% nchini Tanzania.

Dr. Paulina Chale kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili alisema idadi ya watu wanaougua magonjwa ya mfumo wa hewa ni kubwa yakiwemo yanayosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa kwa muda mrefu.

Waziri wa Nishati, January Makamba alisema atasimamia na kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Rais ili kutimiza lengo la serikali ifikapo mwaka 2032 kila kaya wapike kwa kutumia Nishati safi.