Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

SERIKALI YAAHIDI KUJENGA VITUO...

SERIKALI YAAHIDI KUJENGA VITUO 15 VYA KUPOZA UMEME.

SERIKALI YAAHIDI KUJENGA VITUO 15 VYA KUPOZA UMEME.

Na Godfrey Mwemezi, Dodoma.

Serikali inaendelea na mchakato wa kujenga vituo vya kupoza umeme katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Vituo 15 vya kupoza umeme vinatarajiwa kujengwa kwa mwaka 2022/2023 na vipo kwenye mpango wa gridi imara, ambapo taratibu za kuwapata wakandarasi wajenzi wa vituo hivyo zinaendelea.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato alipokuwa akizungumza kwenye semina ya wabunge wa kamati ya Nishati na Madini na kamati ya PAC iliyofanyika katika ukumbi wa Jeongo la Osha Jijini Dodoma, Septemba 24, 2022.

Alisema serikali imetenga sh. bilioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya kupoza umeme katika wilaya ya Mkuranga, Tunduru, Mpanda, Mlele, Sikonge, Uvinza, Urambo, Ngara, Handeni, Bariadi, Ukerewe, Lushoto, Rombo, Kilindi na Kishatu ambapo ujenzi wa vituo hivyo utaanza mwezi Oktoba mwaka huu.

Byabato alisema Shirika la Umeme nchini (TANESCO) limefanya upembuzi yakinifu na kubaini maeneo yenye mahitaji makubwa ambayo vituo hivyo vya kupoza umeme vitajengwa.

"Serikali imezingatia zaidi maeneo yenye changamoto kubwa ya upatikanaji wa umeme wa uhakika na hivyo Wizara tumeamua kuanza na hayo ili wananchi wapate umeme wa uhakika," alisema Byabato.

Alisema kuwa mwaka 2023/2024 TANESCO itaendelea kujenga vituo vya kupoza umeme kupitia mpango wake wa gridi imara katika maeneo yenye mahitaji ya kati ambayo hayakufikiwa katika awamu ya kwanza ya mradi.

"Lengo la Serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha kila mtanzania mwenye uhitaji wa kupata huduma ya umeme anafikiwa na huduma hiyo," alisema Byabato.

Pia Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhe. Felchesmi Mramba, alisema kuwa serikali inaendelea na mikakati mbalimbali ili kuhakikisha inasimamia vyanzo vya kuzalisha umeme ukiwemo mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) pamoja na Ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha chalinze ambacho Ujenzi wake unaendelea vizuri.

Kadhalika Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya Nishati na Madini Dunstan Kitandula, alishauri serikali kuongeza usimamizi wa ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa maji ya Julius Nyerere ili uweze kukamilika kwa wakati kutoka na umuhimu wa mradi huu kwa taifa.

" Pamoja na hilo, kuna suala la utunzaji wa mazingira japo kuna wahusika wa jambo hili lakini nyie kama wenye mtoto wa mradi huu mnaangalie uwezekano wa utengenezaji na utunzaji wa mazingira na kuhakikisha mnatunza vyanzo na kuja na mkakati wa kupanda upya miti kwenye maeneo yaliyoaribiwa." Alisema Dunstan Kitandula Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Nishati na Madini.

Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya Nishati na Madini Dunstan Kitandula, akitoa ushauri kwa wizara ya nishati wakati wa semina ya wabunge wa kamati ya kudumu ya Nishati na Madini na kamati ya PAC, iliyofanyika katika ukumbi wa jengo la OSHA, 24 Septemba, 2022 Jijini Dodoma.