The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

TANZANIA, NORWAY KUIMARISHA US...

TANZANIA, NORWAY KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA NISHATI

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema Tanzania na Norway zinaendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta ya nishati kupitia uwekezaji, maendeleo ya miundombinu, teknolojia, mafunzo ya wataalamu na matumizi ya nishati endelevu ili kuongeza fursa za maendeleo na kuimarisha usalama wa nishati nchini.

Dkt. Homera ameyasema hayo Novemba 20, 2026, alipokutana na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Tone Tinnes, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam, ambapo wamejadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano.

Amesema Tanzania inathamini ushirikiano na Norway uliodumu kwa zaidi ya miaka 50 na kuchangia maendeleo ya miundombinu ya nishati, taasisi na rasilimali watu kupitia misaada ya kifedha, kiufundi na kitaasisi.

Akieleza mchango huo, Dkt. Homera ametaja tafiti za upembuzi yakinifu wa Mradi wa Stiegler’s Gorge zilizofanyika miaka ya 1970 na 1980, zilizoweka msingi wa Mradi wa Julius Nyerere wenye uwezo wa MW 2,115, pamoja na miradi ya Mtera (MW 80) na Kihansi (MW 180).

Ametaja pia ushirikiano katika mafunzo kupitia Norad Fellowship Programme, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Norwegian University of Science and Technology (UDSM–NTNU), pamoja na programu za kukuza uwezo wa wataalamu, wakiwemo wanawake wahandisi.

Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kufikisha upatikanaji wa umeme kwa asilimia 100 ifikapo 2030, matumizi ya nishati safi ya kupikia asilimia 75 ifikapo 2030 na kuongeza mchango wa nishati jadidifu katika uzalishaji umeme hadi asilimia 75 ifikapo 2030.

Katika uwekezaji, amezikaribisha kampuni za Norway kushiriki katika miradi ya uzalishaji umeme kupitia PPP, IPP na EPC+F, pamoja na miundombinu ya usafirishaji umeme, uboreshaji wa gridi, mifumo ya kuhifadhi nishati na teknolojia za kuunganisha nishati jadidifu.

Katika mafuta na gesi asilia, amependekeza ushirikiano katika utafutaji na uzalishaji, usafirishaji na usambazaji, matumizi ya gesi ikiwemo CNG, viwanda vya petrochemical, ushirikishwaji wa wazawa, uhamishaji wa teknolojia na mafunzo. Pia amesisitiza usimamizi wa mazingira na kupunguza uzalishaji wa methane.

Kuhusu jotoardhi, ameeleza umuhimu wa ushirikiano katika tafiti, tathmini ya rasilimali, upembuzi yakinifu, uwekezaji na mafunzo ili kuongeza vyanzo vya umeme.

Akizungumzia nishati safi ya kupikia, Dkt. Homera amesema Wizara inaandaa mpango wa kuwapatia vijana 1,840 kutoka halmashauri 184 mafunzo ya kutengeneza majiko banifu, huku Serikali ikiandaa mikopo kwa ajili ya kuwawezesha kuendeleza shughuli hizo.

Kwa upande wake, Balozi Tinnes amesema Norway inaendelea kushirikiana na Tanzania kwa kufadhili na kuwekeza katika miradi ya umeme, nishati jadidifu, mafuta na gesi asilia, pamoja na kukuza viwanda na uhamishaji wa teknolojia.