Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA...

​TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA PETROLI WA AFRIKA MASHARIKI KWA MAFANIKIO

TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA PETROLI WA AFRIKA MASHARIKI KWA MAFANIKIO

Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa Nishati wameshiriki Maonesho na Mkutano wa Kumi (10) wa Petroli wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’23) ambapo Tanzania ilifanikiwa kutangaza fursa za uwekezaji na ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi asilia.

Mkutano huo uliofanyika Kampala, nchini Uganda kuanzia tarehe 9 – 11 Mei, 2023, ulishirikisha nchi saba za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Makatibu Wakuu wa nchi husika walieleza maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi na kutangaza fursa za uwekezaji katika nchi zao kwa wadau mbalimbali walioshiriki Mkutano huo zikiwemo Kampuni za Kimataifa za mafuta na gesi, mabenki, kampuni za kodi, bima na watoa huduma mbalimbali.

Kwa upande wa Tanzania Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba alieleza kuhusu fursa hizo zinazopatikana nchi Tanzania na kukaribisha wawekezaji nchi kuja kuendeleza rasimali ya mafuta na gesi.

Ujumbe wa Tanzania ulijumuisha viongozi mbalimbali wakiwemo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Dunstan Kitandula; Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Prof. Mark Mwandosya; Mwenyekiti wa Bodi za PURA, Halfani R. Halfani pamoja na wakuu wa Taasisi na wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha na Mipango, Taasisi za Serikali na wawekezaji kutoka sekta binafsi.

Mkutano huo pia ulijadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya mafuta na gesi hususan mjadala unaoendelea wa kuhamia katika nishati safi (Energy Transition). Hivyo, Mkutano uliazimia matumizi ya nishati safi na uendelezaji bora wa rasilimali za mafuta na gesi kwa kutumia teknolojia za kisasa kwa lengo la kuhakikisha uwepo na upatikanaji wa nishati ya kutosha na endelevu kwa kuzingatia usalama wa mazingira.

Kwa mujibu wa makubaliano ya nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mikutano kama hii hufanyika kila baada ya miaka miwili kwa kupokezana baina ya nchi Wanachama. Hivyo, Tanzania ilitumia Mkutano huo kuongeza uzoefu katika kujiandaa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kumi na Moja (11) wa Petroli wa Afrika Mashariki (EAPCE’25) unaotarajiwa kufanyika nchini Tanzania.