Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Tanzania, Zambia kushirikiana...

​Tanzania, Zambia kushirikiana katika umeme, mafuta na gesi.

Tanzania, Zambia kushirikiana katika umeme, mafuta na gesi.

Na Timotheo Mathayo, Dar es Salaam.

Mawaziri wa Nishati kutoka Zambia na Tanzania wamekutana kwa ajili ya kuzungumzia maendeleo ya sekta ya Nishati kati ya Nchi hizo mbili zenye historia ya kuwa na mahusiano mazuri ya kidiplomasia.

Kikao hicho kimefanyika leo Jumatatu katika ukumbi wa Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam ambapo kimejumuisha wataalam kutoka Tanzania na Zambia, kimejadili masuala mbalimbali yaliyopo kwenye sekta ya Nishati kati ya mataifa haya.

Waziri wa Nishati wa Tanzania, January Makamba amesema Tanzania imejenga kituo cha kusafirisha umeme kwenda Mikoa ya nyanda za juu kusini pamoja na kituo cha kuunganisha umeme kupeleka Zambia.

Amesema kuwa wamejadiliana kuhusu Mradi wa umeme unaoingia kutoka Zambia kuja Sumbawanga Mkoani Rukwa nchini Tanzania pamoja na changamoto zake.

Mawaziri hao wamezungumza juu ya biashara ya uingizaji na uagizaji wa mafuta kwa sababu Zambia kwa sehemu kubwa inaingiza nishati ya Mafuta kupitia bandari za Tanzania.

Kuhusu changamoto ya bei ya Mafuta katika nchi zao wamekubaliana kutafuta njia bora ya kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.

Makamba amesema lengo la ziara ya Waziri wa Nishati wa Zambia ilikuwa ni kutembelea Mradi wa Bomba la mafuta la Tanzania na Zambia (TAZAMA) lililojengwa miaka ya 1960.

Waziri wa Nishati wa Zambia, mhandisi Kapala amesema nchi yake ipo katika maandalizi ya kuingia katika mfumo wa biashara ya umeme katika nchi za kusini mwa Afrika ambapo Tanzania imepiga hatua kubwa.

Awali Bomba hili lilikuwa likisafirisha Mafuta ghafi kutoka Tanzania kwenda Zambia ambayo kwa kipindi hiki Mafuta hayo hayaagizwi, hivyo Zambia wanatumia Mafuta ya dizeli.

Bomba la TAZAMA ni ubia kati ya nchi mbili ambapo Tanzania inamiliki asilimia 33 na Zambia ina umiliki wa asilimia 66, hivyo kuna mkakati wa kubadili mfumo wa Bomba hili ili lisafilishe mafuta ya dizeli.

Katika kikao hicho Mawaziri hao wamezungumzia Tanzania kuiuzia gesi Zambia pale itakapoanza kuzalisha gesi kutoka kwenye visima vilivyopo kwenye bahali kuu.

Hata hivyo walizungumzia suala la ulinzi wa Bomba la TAZAMA mara tu litakapoanza kusafirisha dizeli na wamekubaliana na kuteua kamati ya wataalam kutoka nchi hizo mbili.