The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

TUME YA UTUMISHI WA UMMA YAIPA...

TUME YA UTUMISHI WA UMMA YAIPA KONGOLE WIZARA YA NISHATI KWA KUZINGATIA SHERIA, KANUNI.

Tume ya Utumishi wa Umma imeipongeza Wizara ya Nishati kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza Utumishi wa Umma katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku.

Pongezi hizo zimetolewa Septemba 14, 2026, na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Ndg. Omari Kitenge, wakati wa kikao kati ya Tume hiyo na Menejimenti ya Wizara ya Nishati iliyoongozwa na Mwakilishi wa Makatibu Wakuu, Bw. Petro Lyatuu, kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati, Mtumba jijini Dodoma.

Kikao hicho kililenga kuhitimisha zoezi la Ukaguzi wa Uzingatiaji wa Sheria katika Utumishi wa Umma (Exit Meeting), lililofanywa na Tume hiyo katika Wizara ya Nishati.

Aidha, Wizara imepongezwa kwa kufanyia kazi hoja zote zilizoainishwa na Tume katika ukaguzi wa mwaka 2023, hatua inayoonesha utayari wa Wizara katika kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia miongozo na taratibu za Utumishi wa Umma na hivyo kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Lyatuu aliwashukuru watendaji wa Tume ya Utumishi wa Umma kwa kufanya ukaguzi huo, akieleza kuwa unaisaidia Wizara kubaini maeneo yenye changamoto na kuyafanyia kazi ili kuhakikisha utekelezaji wa majukumu unaendelea kwa kuzingatia miongozo na taratibu zinazoongoza Utumishi wa Umma.