Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​TUNAENDELEA KUBORESHA MIUNDOM...

​TUNAENDELEA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA UMEME ILI WANANCHI MPATE UMEME WA UHAKIKA- MHE.SALOME

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha miundombinu ya umeme nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika.

Mhe. Salome ameyasema hayo Novemba 11, 2025 Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kukagua Vituo vya kufua umeme kwa njia ya gesi vya Kinyerezi na Ubungo.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya umeme nchini kwa kutekeleza miradi mipya ya kuzalisha umemei kupitia gesi asilia ili kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo kwa wananchi.

Amesema mradi mpya wa kuzalisha umeme kwa gesi katika kituo cha Kinyerezi utakuwa na mchango mkubwa kwa wakazi wa Gongo la Mboto na Mbagala, ambao wamekuwa wakitegemea umeme kwa shughuli za viwanda na biashara.

“Uzalishaji wa umeme kwa njia ya gesi Kinyerezi utayapa maeneo ya Mbagala na Gongo la Mboto umeme wa uhakika kwani maeneo haya yana watu wengi na viwanda vingi hatahivyo mpaka sasa transfoma ya MVA 120 imeshafungwa na majaribio yameanza hivyo itaboresha upatikanaji wa umeme majumbani na viwandani kwa wananchi wa maeneo hayo. Amesema Mhe. Salome

Mhe. Salome amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika Sekta ya umeme kwani utekelezaji wa miradi hiyo yote ya umems inalenga kuhakikisha Watanzania wanapata nishati bora, ya uhakika na yenye kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya umeme lakini pia kwa kuhakikisha waendesha mitambo hiyo ni wazawa hivyo kuongeza ujuzi wa ndani na kupunguza gharama za uendeshaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Lazaro Twange ameeleza kuwa miradi hiyo ina manufaa makubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam, kwani inaboresha uwezo wa miundombinu kuendana na ongezeko la mahitaji ya kila siku huku akisisitiza kuwa kutokana na uzalishaji wa umeme katika kituo cha Kinyerezi wananchi wameendelea kupata umeme wa uhakika na wakudumu katika matumizi ya majumbani na viwandani.