Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

UCHIMBAJI GESI KITALU CHA RUVU...

UCHIMBAJI GESI KITALU CHA RUVUMA UKAMILIKE KWA WAKATI-MAKAMBA

UCHIMBAJI GESI KITALU CHA RUVUMA UKAMILIKE KWA WAKATI-MAKAMBA

Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba, ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA),
kuhakikisha mradi wa uchimbaji wa gesi kitalu cha Ruvuma kilichopo mkoani Mtwara
unakamilika kwa wakati.

Mhe. Makamba aliyasema hayo tarehe 25/11/2022 jijini Dar es Salaam wakati
wa hafla ya uwekaji saini Mkataba wa Nyongeza wa Uzalishaji na Ugawanaji Mapato (PSA)
Kitalu cha Ruvuma-Mtwara kati ya Wizara ya Nishati, TPDC, Kampuni ya ARA
Petroleum na Kampuni ya Ndovu Resources.

‘’Dhamira ya Serikali ni kuona mradi huo unakamilika ndani ya miezi 12 hadi 18 na
hatutegemei kusikia mradi huo unachelewa kutokana na changamoto ya fedha.Mradi
huo ukikamilika utakuwa mradi wa kwanza wa gesi ambao utalinufaisha Taifa katika
nyanja mbalimbali ikiwemo Serikali kupata Mrabaha (12.5%) , kupata kodi, Serikali
kupata gawio la mapato yatokanayo na mauzo ya gesi pia ajira kwa wananchi wa
Mikoa ya Lindi na Mtwara.” Alisema Mhe. Makamba

Waziri Makamba aliongeza kuwa, “pia eneo la Lindi, Serikali imeamua kujenga Chuo (Polytechnic) cha Masuala ya Mafuta, Gesi na Umeme, ili kujengea watu wetu uwezo, lakini pia tutajenga Special Economic Zone ndani ya eneo la mradi ili kuchochea maendeleo ya Lindi na Mtwara baada ya mradi kukamilika.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio alisema utafiti na ugunduzi wa gesi ulishafanyika na kinachofanyika sasa hivi ni kuanza kwa ujenzi wa bomba la gesi kutoka eneo la
Ntorya hadi Madimba na baada ya kukamilika kwa ujenzi huo uzalishaji wa gesi
utaanza.

Dkt. Mataragio alisema kuwa, uwekezaji huo wenye thamani ya Dola za Kimarekani
milioni 500 unatarajiwa kuzalisha takribani futi za ujazo trilioni 1.6 ambacho ni kiasi cha
gesi kilichogunduliwa katika eneo hilo na kuweka wazi kuwa utekelezaji wake utasaidia
kuongeza chachu na wawekezaji wengi zaidi.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya ARA Petroleum (Tanzania), Ndg. Erhan Saygi
aliishukuru Serikali ya Tanzania hususan viongozi wa Serikali za Vijiji kwa ushirikiano
waliouonyesha na kuongeza kuwa, kukamilika kwa mradi kutachagiza uboreshaji wa
miundombinu na kuongeza ajira ili kukuza pato la wananchi na Taifa kwa ujumla.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na vongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bi.
Zainab Telack, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed pamoja na
Wabunge wa Mikoa ya Lindi na Mtwara.