The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

UJUMBE SAHIHI UTAHARAKISHA MAT...

UJUMBE SAHIHI UTAHARAKISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA.

Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia, Bw. Nolasco Mlay, amesema utoaji wa ujumbe sahihi na wenye uelewa wa pamoja kwa wananchi utaharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, kwani jamii itakuwa na taarifa sahihi zitakazoiwezesha kufanya maamuzi ya kutumia teknolojia mbalimbali za nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi ya kupikia (LPG), umeme, biogesi, gesi asilia na mkaa mbadala.

Bw. Mlay amebainisha hayo Julai 14, 2026 wakati akiongea katika Warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari, Maafisa Mawasiliano Serikalini wa Mikoa, Taasisi, Wizara pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati kuhusu uandishi na uhamasishaji wa masuala ya nishati safi ya kupikia inayofanyika katika Ukumbi wa Morena Hotel mkoani Morogoro.

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kuhakikisha ifikapo 2034 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.

Amefafanua kuwa, baada ya uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi yaNishati Safi ya Kupikia uliofanywa mwaka 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwaka 2025 Serikali ilizindua pia Mkakati wa Mawasiliano utakaowezesha kufikisha ujumbe mmoja na sahihi kwa jamii kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Amesema mkakati huo wa mawasiliano unalenga kuhakikisha wadau wote wanaohusika na utoaji wa elimu wanakuwa na uelewa wa pamoja ili kuwasilisha taarifa sahihi na zenye kuhamasisha wananchi kufanya uchaguzi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa manufaa ya kuboresha afya na kulinda maziringira.

Amesisitiza kuwa wanahabari ni wadau muhimu katika kufanikisha mkakati huo, kwani kupitia wanahabari wanachi watapata ujumbe sahihi na vyombo vya habari vitafikisha ujumbe sahihi kwa Watanzania wengi zaidi, jambo litakaloongeza uelewa wa jamii na kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Amesisitiza kuwa wanahabari na maafisa habari ni wadau muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa Mkakati wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia, kwani kupitia utoaji wa taarifa zenye usahihi na zinazozingatia ujumbe wa pamoja utasaidia kuongeza uelewa wa jamii, kuondoa upotoshaji na kuharakisha kufikiwa kwa malengo ya taifa ya kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia.