Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Wabunge wapata elimu ya Nisha...

​Wabunge wapata elimu ya Nishati Safi ya Kupikia

Wabunge wapata elimu ya Nishati Safi ya Kupikia

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamepata elimu kwa kina ya nishati safi ya kupikia ambayo imejumuisha pia Rasimu ya Dira ya Taifa ya Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia na Mpango Mkakati wa utekelezaji wake lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033.

Wabunge hao wamepata elimu hiyo tarehe 27 Mei, 2023 jijini Dodoma katika Semina iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kuongozwa na Waziri wa Nishati,

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema kuwa takriban asilimia 85 ya watanzania wanatumia nishati ya Tungamotaka ambayo inajumuisha kuni, mikaa, magogo, mabaki ya mazao na vinyesi vya wanyama ambapo asilimia 72 ya nishati yote nchini inatumika majumbani na si viwandani au katika usafirishaji.

“Asilimia kubwa ya nishati inayotumiwa na watanzania ni tungamotaka na inatumika majumbani kwa kupikia kwa hiyo kuzungumzia tu mitambo ya kuzalisha na kusafirisha umeme, gesi au mafuta haitoshi kwani watanzania wengi wanatumia nishati ya kupikia ambayo ni ya tungamotaka hivyo ili kutendea haki kazi tulizopewa tumeona lazima tuingilie kati kwenye nishati safi ya kupikia na hilo ndio chimbuko la kulipa nguvu suala hili.”amesema Makamba

Waziri wa Nishati alitaja athari mbalimbali zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo salama ikiwemo ya vifo takriban 33,000 kwa mwaka vinavyotokana na magonjwa ya mfumo wa kupumua unaotokana na moshi wa nishati isiyosafi kwa kupika, athari za mazingira kutokana na ukataji wa kuni na uchomaji wa mkaa pamoja na athari za kijamii.

“ Suala la nishati safi ya kupikia ni utekelezaji wa Sera ya Nishati ya mwaka 2015 ambayo inasema kwamba Serikali itachukua hatua mahsusi za kuwasaidia watanzania ili wahame kutoka kwenye nishati isiyo safi na salama kwenda kwenye nishati ya kisasa na safi, hivyo hapa tunatekeleza Sera ya Nishati .”Amesema Makamba

Amesisitiza kuwa, utekelezaji wa Nishati Safi ya Kupikia unalenga kuleta ustawi wa kinamama na watanzania na si nadharia na ndio maana Serikali imelibeba kwa nguvu kubwa suala hili ambapo aliongeza kuwa asilimia tano tu ya watanzania kwa sasa ndio wanatumia nishati safi ya kupikia.

Akizungumzia kuhusu matumizi ya gesi ya mitungi, amesema kuwa ni salama.

Waziri Makamba ametoa wito kwa wabunge kuhamasisha wananchi kutumia nishati hiyo na kuwapatia Wabunge vocha za mitungi ya gesi 100 kila mmoja lengo likiwa ni kusaidia kuhamasisha kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuwa mitungi ya gesi ya kupikia ni salama wananchi wasihofu kuitumia.

Katika hatua nyingine, Waziri Makamba amewakaribisha Wabunge hao katika Maonesho ya Wiki ya Nishati yatakayoanza tarehe 29 Mei hadi tarehe 01 Juni, 2023 katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma na kueleza kuwa, Maonesho hayo pia yatatumika kutoa taarifa ya miradi mbalimbali ya nishati na kutoa utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazohusu Sekta kwani viongozi Wakuu wa Wizara pamoja na Taasisi watakuwepo katika Maonesho hayo.

Katika Semina hiyo pia wabunge walipata uelewa zaidi kuhusu hali ya upatikanaji umeme, utekelezaji wa miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme pamoja na usambazaji wa nishati safi ya kupikia katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wao, Wabunge hao wakiongozwa na Mhe.Dunstan Kitandula ambaye alimwakilisha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamepongeza kwa semina hiyo ambayo imewapa uelewa wa utekelezaji wa miradi mbalimbali na walitoa maoni mbalimbali yatakayofanyiwa kazi na Wizara.

Waziri Makamba aliambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athuman Mbuttuka ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na viongozi wengine wa Wizara ya Nishati, REA na TANESCO.