WANAHABARI WATAKIWA KUANDAA VIPINDI NA HABARI ZA KUSHAWISHI ZINAZOCHOCHEA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA.
Mkurugenzi wa Huduma za Redio kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Bi. Anna Kwambaza, amewataka Wanahabari kuandaa vipindi na habari zenye uwezo wa kushawishi na kubadili mitazamo ya wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Bi. Kwambaza ametoa wito katika Warsha ya Kuwajengea Uwezo Waandishi wa Habari pamoja na Maafisa Mawasiliano wa Serikali kuhusu Uandishi na Uhamasishaji wa Masuala ya Nishati Safi ya Kupikia iliyofanyika mkoani Morogoro mara baada ya kuwasilisha mada ya Ukuzaji wa Habari za Nishati Safi ya Kupikia, iliyojumuisha namna ya kubuni na kuwasilisha mawazo ya habari kuhusu nishati safi ya kupikia, kuandika vichwa vya habari vinavyovutia na kupokea maoni ya kuboresha kazi hizo, ambapo baadaye aliwapa washiriki nafasi ya kuandaa vichwa vya habari, habari, vipindi vya redio na televisheni pamoja na simulizi kuhusu nishati safi ya kupikia na kuviwasilisha katika makundi kwa ajili ya kujadiliwa na kupatiwa mrejesho.
Katika mafunzo hayo, Bi. Kwambaza aliwaelekeza washiriki namna ya kuandaa vipindi vya redio na televisheni vinavyovutia wasikilizaji na watazamaji, kuandika habari zenye mvuto pamoja na kutengeneza simulizi zinazoibua uelewa na kuhamasisha jamii kuchukua hatua ya kutumia nishati safi ya kupikia.
Sambamba na hilo aliwafundisha namna ya kuibua mawazo ya habari, kuandika vichwa vya habari vinavyovutia na kuwasilisha mawazo ya habari kwa ufanisi.
Baada ya mafunzo hayo, washiriki walipata nafasi ya kufanya mazoezi kwa kuandaa vipindi vya redio na televisheni, kuandika simulizi na habari kuhusu nishati safi ya kupikia, kisha kuwasilisha kazi zao mbele ya wenzao kwa ajili ya kujadiliwa na kupata mrejesho kutoka kwa mkufunzi.
Akitoa maoni kuhusu kazi zilizowasilishwa, aliwasisitiza washiriki kuhakikisha wanawafahamu walengwa wa maudhui wanayoandaa ili yaweze kubadili mitazamo na kuwahamasisha wananchi kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.
Alifafanua kuwa kila kipindi, habari au simulizi inapaswa kuwa na lengo linaloeleweka, liendelee kumvutia msikilizaji au msomaji hadi mwisho, lijibu maswali muhimu anayoweza kuwa nayo na litumie lugha nyepesi inayoeleweka kwa wananchi.
Aidha, aliwataka waandishi wa habari na Maafisa mawasiliano Serikalini kuhakikisha wanatengeneza vipindi na simulizi vinavyoshawishi badala ya kutoa taarifa pekee, akisisitiza kuwa maudhui bora ni yale yanayomwezesha mwananchi kuelewa, kuamini na hatimaye kubadili tabia kwa kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.