WANANCHI MILIONI 1.7 KUNUFAIKA NA UMEME KILA MWAKA KUPITIA USHIRIKIANO WA TANESCO NA CRDB – SALOME.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema kuwa takribani Watanzania milioni 1.7 wanatarajiwa kunufaika kwa kupata huduma ya umeme kila mwaka kupitia mpango wa kuharakisha uunganishaji wa umeme katika kaya unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Benki ya CRDB.
Amesema mpango huo ni muhimu katika kuongeza kasi ya upatikanaji wa umeme nchini, huku ukiwezesha wananchi wengi zaidi kuunganishwa na huduma hiyo muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mhe. Salome ameyasema hayo leo, Novemba 23, 2026, katika ukumbi wa Kilimanjaro Hotel (Hyatt Regency) wakati wa Semina ya Uzoefu kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, iliyotolewa na CRDB kwa kushirikiana na TANESCO, kwa lengo la kuwajengea wajumbe uelewa kuhusu mpango wa uharakishaji wa uunganishaji wa umeme katika kaya.
Aidha, ameeleza kuwa mpango huo ni chachu muhimu katika kufikia malengo ya Mpango wa Mission 300, unaolenga kuhakikisha wananchi milioni 300 barani Afrika wanapata huduma ya umeme.
Semina hiyo imehudhuriwa pia na wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, pamoja na wadau wengine wa sekta ya nishati.