Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​WIZARA YA NISHATI YAANZA KUTE...

​WIZARA YA NISHATI YAANZA KUTEKELEZA MAAGIZO YA RAIS

WIZARA YA NISHATI YAANZA KUTEKELEZA MAAGIZO YA RAIS

Na Timotheo Mathayo, Dar es salaam

Waziri wa Nishati, January Makamba alisema kuwa wizara yake imeanza utekelezaji wa agizo la Rais alilotaka taasisi zote za umma na binafsi zenye watu zaidi ya 300 kupika kwa kutumia Nishati safi.

Makamba ametoa kauli hiyo Jumatano ya Novemba 03, 2022 wakati alipokuwa anafunga mjadala kuhusu Nishati safi ya kupikia uliofanyika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es salaam.

Kufuatia agizo hilo lililotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan siku ya Jumanne Novemba 01, 2022 kuhusu taasisi hizo kuacha matumizi ya kuni na mkaa, wizara imeanza kuchukua hatua.

Makamba alisema kuwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ashirikiane na wizara nyingine waweze kuorodhesha taasisi zilizo chini yao zenye watu zaidi ya 300 kwa ajili ya kuanza matumizi ya Nishati safi ya kupikia.

Alisema serikali na wadau wengine wapo katika mchakato wa kusambaza mitungi ya gesi kila eneo nchini ili iwe rahisi kuwafikia wananchi.

"Serikali imetoa sh. bilioni 6 kwa shirika la maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) ili waendelee na kazi za kusafirisha na kusambaza gesi kutoka Mtwara," alisema Makamba.

Makamba ametoa mwito kwa wawekezaji na wasambazaji wa gesi majumbani kujitokeza na kufanya kazi hiyo ili lengo la serikali litimie haraka.

Mkurugenzi wa (REA) Mha.Hassan Seif Said kutoka Wakala wa Nishati vijijini ameahidi kwamba watashirikiana na TPDC kusambaza nishati safi ya kupikia ili iwafikie wakazi wengi wanaoishi katika maeneo ya vijijini.