WIZARA YA NISHATI YAKARIBISHA WANANCHI KUTEMBELEA BANDA LAKE MAONESHO YA NANENANE DODOMA.
Wizara ya Nishati inashiriki Maonesho ya Wakulima (NANENANE) yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Kupitia maonesho hayo, Wizara inaonesha namna sekta ya nishati inavyochangia kuongeza tija katika kilimo kupitia upatikanaji wa umeme hasa maeneo ya vijijini, matumizi ya nishati safi ya kupikia na teknolojia nyingine za kisasa zinazochochea maendeleo endelevu na kulinda mazingira.
Aidha, ushiriki wa Wizara unalenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu nafasi ya nishati katika kuboresha uzalishaji wa kilimo, kuongeza thamani ya mazao na kuinua ustawi wa wakulima.
Maonesho haya yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha sekta ya kilimo na nishati kwa ajili ya maendeleo jumuishi ya kijamii na kiuchumi.
Katika maonesho ya NaneNane Wizara ya Nishati ipo pamoja na taasisi zake ambazo ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Wakala wa Nishati Vijijimi (REA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).
Maonesho ya Nanenane mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: "Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050."
Karibu Banda la Wizara ya Nishati!